Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Mfuko wa Pembejeo

AGITF Logo
Historia ya AGITF

Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (ambao hapa utaonekana kama "Mfuko") ulianzishwa chini ya Sheria ya Mfuko wa Pembejeo za Kilimo, Sura ya 401, Marekebisho ya 2002, kwa lengo la kupunguza pengo la usambazaji wa pembejeo kwa kufadhili uagizaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo.

Sababu kuu za kuanzishwa kwake ni mabadiliko ya Sera ambayo yanajumuisha:

  1. Kubadilisha Sera zinazohusiana na biashara za pembejeo na zana za kilimo kutoka kuwa zinazoendeshwa na serikali hadi sekta binafsi
  2. Kubadilisha majukumu na kanuni za Bodi za Mazao, hali iliyosababisha kushindwa kuwezesha upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo
  3. Kufutwa kwa ruzuku za pembejeo na zana za kilimo kama vile mbolea na dawa za kuua wadudu wa mifugo.

Mfuko wa Pembejeo ulionekana kama njia mbadala ya kufadhili ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa pembejeo kwa wakulima.

 

MADHUMUNI YA KUANZISHWA KWA MFUKO

  1. Kutoa mikopo (to finance) kwa kadri ya masharti na vigezo vitakavyowekwa na Bodi pamoja na kugharamia uagizaji na usambazaji wa pembejeo nchini.
  2. Kugharamia huduma za ushauri elekezi au msaada wowote wa kitaalamu kuhusiana na upatikanaji, usambazaji na matumizi ya pembejeo za kilimo.
  3. Kulipia gharama za uendeshaji wa Mfuko.

 

KAZI ZA BODI YA WADHAMINI

  1. Kumshauri Waziri kuhusu Sera ya Mfuko na kusimamia utekelezaji wake
  2. Kutambua mahitaji ya kitaifa ya Pembejeo za Kilimo na kujua gharama zake
  3. Kusaidia upatikanaji wa fedha za kugharamia ununuzi na usambazaji wa pembejeo za kilimo
  4. Kusimamia utoaji, usambazaji na uhifadhi wa pembejeo za kilimo kwa wakati
  5. Kusimamia matumizi ya fedha za Mfuko kwa mujibu wa kanuni bora za kifedha
  6. Kutoa mikopo kwa kuzingatia kanuni za msingi na urejeshaji wa mikopo na riba yoyote inayolipwa kwa mkopo wowote
  7. Kumtaarifu Waziri mara kwa mara kuhusu hali ya pembejeo nchini na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuzinunua na;
  8. Kushirikiana na Taasisi au Mamlaka zinazohusika na ufuatiliaji na usimamiaji wa viwango au ubora wa bidhaa ili kuhakikisha kuwa pembejeo za kilimo zinazoingizwa kwa mkopo kutoka Mfuko wa Pembejeo ni za kiwango au ubora unaokubalika.

 

WALENGWA WA MFUKO

  1. Wakulima mmoja mmoja au vikundi (Registered farmer groups/Water user association)
  2. Taasisi binafsi na za Umma
  3. Benki za kijamii na;
  4. Vyama vya Ushirika (SACCOS, AMCOS).